Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. 

Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo letu tutakwenda kujifunza jinsi ya kumfundisha mtoto kuvua samaki.

Rafiki, wazazi wa siku hizi wamekuwa ni wazazi wa kukwepa majukumu yao. Waswahili wanasema kuzaa siyo kazi ni kulea mwana, nami ninakubaliana na wa swahili wanavyosema. Wazazi wengi wamejisahau sana katika jukumu la malezi kiasi kwamba na watoto wengi wanaishi maisha ya uyatima angali bado wazazi wake wako hai. Watoto wamekuwa ni watu waliokosa mwongozo mzuri hivyo wanakuwa wanajiangalia wenyewe kama vile watoto wa wanyama.

Binadamu ni watu waliopewa utashi mkubwa kuliko viumbe vingine vyote, lakini cha ajabu binadamu huyo huyo amezidiwa na viumbe vingine. Kwa mfano, kama sungura kabla hajazaa huwa anajitoa upendo wa sadaka kwa kutoa manyoya yake kwa ajili ya kutengeneza mazingira ya joto na kumkinga mtoto wake na baridi. Lakini unaweza kumkuta mzazi mwingine hana upendo wa kujitoa sadaka kwa ajili ya mtoto wake na kutawaliwa na ubinafsi wa kujiangalia yeye kama yeye.

Mpendwa msomaji, wazazi wengine wanalalamika mbele ya watoto wao kuwa mimi ninahangaika najinyima kwa ajili ya kukusomesha wewe. Sasa jukumu la mzazi kumsomesha mtoto ni haki yako mzazi na wala haina haja ya mzazi kulalamika. Wewe ndiyo uliyemleta dunia hivyo unapaswa kuingia gharama ya kumhudumia na kumpatia mahitaji yote muhimu bila kulalamika kwa sababu ni majukumu yako. Mtoto haitaji kusikia hadithi zako au malalamiko yako haki ya malezi na kupatiwa mahitaji yake ya msingi ni jukumu la mzazi na mtoto ni haki yake kabisa.

Ndugu, lengo la somo letu la leo ni kutaka kujifunza jinsi ya kumfundisha mtoto kuvua samaki na badala ya kumpa samaki. Kama tunavyojua wazazi wengi wanakosa maarifa ya kuwafundisha watoto wao jinsi ya kuvua samaki badala yake wanapa watoto samaki. 

Unampatia mtoto samaki ujue atamla na hatimaye akiisha atakuomba au kukudai tena. 

Kumbe njia nzuri siyo kumpatia mtoto samaki badala yake ni kumfundisha jinsi ya kuvua samaki kwa kumpa nyavu akavue. Na siku zote ukimfundisha mtoto kujitegemea ni nzuri zaidi kuliko kumfundisha mtoto kukutegemea zaidi.

Kwa mfano, kama mtoto anapenda mayai na huwa unamnunulia mara kwa mara hivyo inakupasa wewe kama mzazi kununua kuku nyumbani na kuanza kumfuga na kumfundisha mtoto jinsi ya kumhudumia vizuri kuku ili azalishe mayai. Kuku ndiyo anakuwa nyavu sasa ya kuvua samaki na mayai yatakayopatikana ndiyo samaki wenyewe. 

Kwa hiyo, kadiri mtoto anavyoweka juhudi kumhudumia kuku vizuri ndivyo na kuku naye atakavyoweza kumzalishia mayai na atapata mayai kulingana na uhitaji wake badala ya kukuomba umnunulie mayai.

Kifupi rafiki yangu, hapa wazazi wanaalikwa kuwafundisha watoto kuzalisha zaidi na siyo kuwapa tu bidhaa. Unatakiwa kumfundisha mtoto kazi kama kuna kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wako na unaweza kukizalisha mfundishe mtoto kuzalisha zaidi. Watoto wakifundishwa kazi tokea wakiwa wadogo inawapa uwezo mkubwa wa kujitegemea kwa maisha yajayo.

Mtoto anayefundishwa kuzalisha anakuwa vizuri zaidi kuliko yule mtoto anayesubiri kupewa samaki. Kama mtoto yuko katika kiwango cha kufundishwa uzalishaji mfundishe kuzalisha siyo kumpa tu samaki. Kama nyumbani una ng’ombe mfundishe jinsi ya kukamua maziwa na kumlisha ng’ombe kuliko kusubiria akamuliwe maziwa na kunywa tu.

Chochote kile kizuri ambacho mzazi unafanya unaalikwa kumfundisha mtoto wako. 

Mfundishe mtoto taaluma yako, mfundishe mtoto kuzalisha, mualike mtoto aone jinsi unavyofanya kazi zako ofisini kwako naye ajifunze. Kama mtoto hajui kupika mfundishe kupika na siyo kumpatia chakula tu, unapomfundisha jinsi ya kupika kitu fulani siku akiwa anauhitaji nacho hawezi tena kukuomba bali ataingia jikoni na kupika. Hata kama mzazi una msaidizi wa kazi nyumbani usimwache mtoto wako akae bure bila kufanya kazi na badala yake apewe majukumu na yeye awajibike.

Kwa hiyo, kadiri unavyompa mtoto mwongozo mzuri akiwa mdogo ndivyo anavyozidi kuwa bora hapo baadaye. Mzazi unaposema hutaki mtoto wako apate shida yaani asifanye kazi unakuwa unamwandalia jeneza la kwenda kumzika mwenyewe kwani utamwandaa kuwa na maisha magumu sana na hatimaye atakuja kushindwa kuwajibika hata pale atakapokuwa na familia yake binafsi. Utakuta majukumu yake binafsi atapenda amwalike mtu mwingine na watoto wanaoandalia vizuri kikazi wanakuwa wazazi wazuri baadaye kwa sababu kama mzazi ni mvivu na mtoto naye atakuwa mvivu.

Hatua ya kuchukua leo, mfundishe mtoto wako jinsi ya kuvua samaki na siyo kumpa samaki. Mfundishe mtoto kazi na kutambua wajibu wake mapema kwa manufaa yake mwenyewe na jamii kiujumla.

Kwa kuhitimisha, tunaalikwa sisi kama wazazi kuwafundisha watoto wetu maadili mazuri na misingi ya kazi tokea wakiwa wadogo. Watoto wanaofundishwa falsafa ya kazi huwa wanakuja kuwa wazuri sana baadaye na wataona kazi ndiyo msingi wa maendeleo yao.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com