Katika vitabu vya dini imeandikwa usimnyime mtoto adhabu lakini sisi tunajifanya kwenda kinyume na vitabu vya dini. Tunawalea watoto wetu utafikiri tutaishi nao milele au kama vile kuna mkataba tuliwahi kuandikishana na watoto wetu kuwa tutakuwa nao milele. Hatutaki wafanye kazi tunataka wakae tu, wengine hatuwafundishi watoto wetu hata namna ya kufanya kazi, kufanya hata usafi wa mwili, mazingira, nguo nakadhalika na tuna waambia wasifanye kazi tumemwajiri mtu wa kufanya kazi hizo.

Huwa tunaona tunaishi usasa kweli, watoto wetu wasipate shida bwana. Wengi wetu hapa wakati tunasoma tuliadhibiwa pale tulipokuwa tunakwenda kinyume au kwenda nje ya mstari na adhabu zilitusaidia kuwa na nidhamu nzuri sana lakini wazazi wa siku hawataki kusikia kuhusu kuwapa watoto wao adhabu. Wazazi wa siku hizi wamekuwa wanasaikolojia wazuri wanakuja na sababu nyingi kwanini watoto wao wasiadhibiwe pale wanapofanya kosa.

raising positive kids

Hata ukimwadhibu mtoto hutoweza kumuua bali utamfundisha tabia lakini kila mtoto anastahili adhabu kiasi kadiri ya umri wake siyo tu kumwadhibu bila sababu. Hakuna haki bila wajibu hivyo kama mtoto anatakiwa kutimiza wajibu wake na mzazi vivyo hivyo anatakiwa kutimiza wajibu wake. Tumekuwa vyanzo vya kuharibu maadili ya watoto wetu sisi wenyewe, tunasingizia tv zinawaharibu watoto wanaangalia mambo yasiyo stahili kwani nani analipia bili ya king’amuzi? Nani aliyenunua hiyo tv? Chochote kinachotokea kwa mtoto mwajibikaji wa kwanza ni mzazi kwani wewe ndiyo uliyealikwa kuwachunga watoto wako kama kuhani.

SOMA; Hii Ndiyo Imani Chanya Unayopaswa Kumjengea Mtoto Katika Malezi.

Usipomwadhibu mtoto wako dunia itakuja kumwadhibu kikatili kabisa. Dunia huwa haina huruma hata wewe mwenyewe ukifanya makosa dunia inakuadhibu, wengine wanaadhibiwa hata kwa riba. Kama unampenda mtoto au watoto wako wafundishe msingi wa maisha, pale anapostahili adhabu mpatie adhabu yake wala usimnyime ni haki yake  lakini unapokataa kumwadhibu unamwandaa kuja kuadhibiwa na dunia na tena dunia ilivyokuwa haina huruma itamwadhibu kikatili, rafiki, mwenye macho haambiwi tazama.

Chanzo cha matatizo mengi katika mahusiano ya ndoa yanaanzia katika malezi. Kama mtoto akilelewa kuwa mama bora atakuwa mama bora vivyo hivyo kwa mtoto wa kiume akilelewa kuwa baba atakuja kuwa baba bora. Maajabu ya siku hizi mtoto wa kike anakatazwa asifanye kazi za nyumbani kisa kuna msaidizi wa kazi, je huyo mtoto wa kike akijakuwa  na familia yake nani atamsaidia majukumu yake? Ndiyo hapo hataria inapoanzia binti anaingia katika maisha ya ndoa hajui hata kupika wala majukumu yake kama mama wa familia hajui, ndiyo hapo hata wengine wanaaumua kuajiri watu kuwasaidia hata majukumu binafsi.

Hatua ya kuchukua leo, mpe adhabu mtoto pale anapostahili kuadhibiwa. Usifiche makosa ya mtoto na ukaogopa kumwadhibu kama hutomwadhibu dunia itakusaidia kumwadhibu tena bila huruma.

SOMA; Huyu Ndiye Adui Namba Moja Kwenye Malezi Ya Watoto.

Kwahiyo, kama unampenda mtoto wako, basi mfundishe misingi ya maisha. Mfundishwe kweli jinsi dunia inavyoenda kadiri ya asili usipindishe ukweli kwani ukipindisha ukweli dunia itamfundisha ukweli kwa adhabu baadaye. Lipia mapema gharama kwa mtoto wako kabla dunia haijamlipia kwa riba kubwa.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku na kupata huduma mbalimbali kama vile vitabu, kwa kutembelea tovuti  hii  hapa  www.mtaalamu.net/kessydeo .

Asante sana na karibu sana !