Chukua mfano uko barabarani, eneo la wavuka kwa miguu, hilo ni eneo kabisa ambalo limetengwa kwa ajili ya wanaotembea kwa miguu. Taa imewaka kuwaruhusu wanaotembea kwa miguu wavuke, na hivyo magari yasimame. Wewe unaanza kuvuka, ghafla inakuja gari na haisimami kama inavyopaswa, inaendelea kuja. Je hapo unafanya nini? Utaendelea kuvuka kwa sababu ni haki yako, au utaacha na kuruhusu gari ipite, japo siyo haki?
Jibu lipo wazi, utaruhusu gari ipite, kwa sababu japo ni haki yako, lakini kama utang’ang’ana kuvuka, utagongwa na hapo utakufa. Hivyo kung’ang’ana kwako na haki, kunayakatisha maisha yako.
Mfano huo uko wazi, kwa sababu unaonesha wazi maisha na kifo, lakini zipo hali nyingi tunazokutana nazo kwenye maisha yetu, ambapo kuna kitu kimetokea, haki iko upande wetu, lakini inabidi tukubaliane nacho kuokoa kitu kikubwa zaidi. Unaweza kung’ang’ana na haki, lakini ukapoteza kitu kikubwa kuliko haki uliyopata.
Hapa nitatoa mifano miwili ambayo tunakutana nayo kila siku;
Moja ni kwenye mahusiano, changamoto nyingi za mahusiano huwa zinatokana na vitu vidogo vidogo sana, labda mmoja amefanya kosa na mwingine anaona kosa hilo ni kubwa na halisameheki, au hata kama atasamehe basi kila wakati atakumbusha. Kwa njia hii mahusiano yanashindwa. Kama aliyefanyiwa kosa angeweka uhai wa mahusiano mbele, mahusiano yangedumu.
Mfano mwingine ni kwenye biashara, kuna wakati kila biashara inatengeneza changamoto kwa wateja wake, au wateja wanajitengenezea changamoto wao wenyewe. Unawauzia kitu na kuwapa maelekezo sahihi, wao wanafanya kinyume na hawapati matokeo sahihi. Mwisho wanarudi kwako na kukulalamikia kwamba ulichowauzia hakifanyi kazi. Sasa hapo kama unataka kukaa upande wa haki, utamsema mteja vibaya na kumwonesha kwamba matatizo ni yake na hapaswi kukulaumu wewe. Lakini kama unataka kuboresha mahusiano na mteja huyo, kuendelea kuwa naye, lazima ukubali malalamiko yake na uwe tayari kumsaidia mpaka atakapopata matokeo aliyokuwa anatarajia kupata alipokuja kununua kwako.
Maamuzi kati ya haki na uhai ni maamuzi yanayohitaji busara kubwa sana kuyafanya, kwa sababu sisi binadamu huwa tunakimbilia kwenye haki, lakini haki mara zote huwa haileti uhai kwenye nyakati ngumu kwetu. Hivyo tujifunze kuweka mlinganyo sahihi kwenye haki na uhai.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante kocha nimekuelewa vizuri sana hata kwenye kupata lazima Kuna vitu utavipoteza hapo kupoteza vitu siyo haki,.
LikeLike
Karibu.
LikeLike
Haki kweli usipotumia mlinganyo inaweza kukuponza, hapo nadhani hekima, busara uvumilivu ni muhimu katika maisha yetu, kufikiri kwa kutumia fikra na sio hisia.
LikeLike
Hakika.
LikeLike
Ni kweli kocha hata humu makazini wengi wameumia na kutesa familia zao kwasababu ya kile wanachokiita kudai haki, nadhani huo mfano wa zebra na gari unawafaa sana.
LikeLike
Asante sana.
LikeLike