2557; Vipimo vya muda.

Sekunde ndiyo kipimo cha chini zaidi cha muda.
Huwa hatuhangaiki sana kuzipima sekunde, isipokuwa kwa mambo yenye ukomo mkali wa muda.
Sekunde chache zinaweza kuleta tofauti kubwa.

Dakika ni kipimo kinachofuatia. Ni kipimo ambacho tunaweza kutumia kufanya mengi, lakini huwa tunakipuuza.
Mfano watu huwa wanalalamika hawana muda wa kusoma vitabu. Lakini unahitaji dakika chache tu kwenye siku yako, zisizozidi kumi kuweza kusoma.
Je kuna mtu anakosa dakika 10 kwenye siku yake?

Saa ni kipimo kilichozoeleka zaidi, hasa kwenye majukumu mbalimbali tunayofanya.
Tunajua kuna masaa 24 tu kwenye siku zetu na hakuna nyongeza. Lakini bado watu hupoteza masaa yao ya siku kwa kufanya mambo yasiyo na tija.

Siku ni kipimo maarufu pia, kuanza na kumalizika kwa siku ni kiashiria cha muda ambao unakwenda.
Kuipangilia siku na kuhakikisha umeitumia vizuri ni hitaji muhimu.

Wiki ni kipimo kinachokusanya siku saba, kipindi kizuri cha kuangalia hatua ambazo mtu unakuwa umepiga kwenye siku hizo.

Mwezi ni kipimo ambacho wengi wamekizoea, kwa sababu ndiyo kinahusika zaidi kwenye malipo.
Ni kipindi cha siku takriban 30 au wili 4. Ni muda unaotosha kufanya mabadiliko makubwa.

Mwaka ni kipimo ambacho huwa tunasisimka nacho zaidi, mwaka kuanza na kuisha huhesabiwa kuwa tukio kubwa. Lakini ni mkusanyiko wa vipimo vyote vya muda tulivyoona hapo juu. Kwenye mwaka unaweza kufanya makubwa sana.

Muongo ni kipimo cha miaka kumi. Huo ndiyo muda unaohitajika ili mtu aweze kufikia ubobezi wa juu kabisa kwenye kitu chochote kile.

Karne ni kipimo cha miaka 100. Miaka ambayo wengi hawaifikii, ila kwa wachache wenye bidhamu ya hali ya juu na wanaotumia vizuri muda wa maisha yao wanafikia.

Milenia ni kipimo cha miaka elfu moja. Hiki ni kipindi ambacho jamii nzima inakuwa imepitia mageuzi makubwa.

Tumekuwa na mazoea ya kudharau vipimo vidogo vya muda na hivyo kuupoteza sana.
Halafu kwa vipimo vikubwa, tunaona muda upo mwingi, nao tunaupoteza pia.

Matokeo yake ni muda unakwenda na hakuna makubwa tunayofanya, tunakuja kushtuka ni ukingoni mwa maisha na hatujayaishi.

Hatua ya kuchukua;
Heshimu na zingatia kila kipimo cha muda. Pangilia kuanzia kipimo cha chini kabisa mpaka cha juu. Kuanzia sekunde mpaka milenia.
Kila unachofanya, fikiria kinaigusaje dubia kuanzia kipimo cha sekunde mpaka kipimo cha milenia.
Kwa namna hiyo utaweza kutumia muda wako vizuri na kwa tija.

Tafakari;
Muda ndiyo rasilimali ambayo tumepewa wote kwa usawa. Tofauti inakuja kwenye namna tunavyoutumia. Kama utashindwa kuutumia muda wako vizuri, hakuna namna unaweza kusaidiwa.

Kocha.