2777; Maji hufuata mkondo wake.

Hii ni kauli rahisi sana ya Waswahili, lakini iliyobeba ujumbe mzito sana.
Ni ujumbe ambao ukiweza kuuelewa utajitenganisha kabisa na mambo yanayokuzuia kufanikiwa.

Kwenye kitabu cha The Richest Man In Babylon ipo hadithi ya bwana mmoja ambaye hakuwa makini na matumizi ya fedha zake.
Alijikuta akiingia kwenye madeni makubwa ambao hakuweza kuyalipa na hivyo kulazimika kukimbia.

Huko alikokimbilia pia mambo hayakwenda vizuri, kwani alijikuta akiuzwa kama mtumwa.
Ni pale aliponunuliwa kama mtumwa ndiyo alimwambia aliyemnunua kwamba yeye hakuzaliwa mtumwa, ni mtoto wa mtu huru.

Jibu ambalo aliyemnunua kama mtumwa alimpatia ndiyo tunajitunza kitu kikubwa sana leo.
Alimwambia utumwa siyo hali ya kuzaliwa, bali ni jinsi mtu alivyo. Kama mtu ana utumwa ndani yake, atakuwa mtumwa hata kama amezaliwa huru. Na kama mtu ana uhuru ndani yake, atakuwa huru hata kama amezaliwa mtumwa. Maji huwa yanafuata mkondo wake.

Tunachojifunza hapa ni kabla hatujahangaika na matokeo ya nje, hebu kwanza tuangalie mkondo wa ndani.
Kinachotokea nje mara nyingi hakina uhusiano na juhudi tunazoweka, bali kina uhusiano na namna tulivyo.

Unadhani kwa nini watu wengi wanaopata fedha nyingi kwa mkupuo huwa wanaishia kuzipoteza zote?
Kwa sababu mkondo wao wa ndani ni wa umasikini, ila nje kumelazimishwa kuwa tajiri.
Kinachotokea ni maji kufuata mkondo wake, hivyo wanapoteza fedha zao na kurudi kwenye umasikini.

Kwenye safari ya mafanikio, watu wengi sana wamekuwa kikwazo kikubwa kwao wenyewe. Wamekuwa wanaweka juhudi kubwa kufanikiwa, ila baadaye wanafanya jambo ambalo linavuruga kabisa mafanikio wanayokuwa wameyapata.

Inaweza kuwa ni kuridhika haraka na kuacha kuendelea kuweka juhudi.
Inaweza kuwa ni kiburi na kuacha kujifunza kwa kuamini tayari wanajua kila kitu.
Au inaweza kuwa ni kulewa sifa na kufanya mambo yaliyo nje ya uwezo.

Haijalishi nini mtu anafanya, matokeo ya mwisho yataamuliwa na mkondo wake, mtazamo mkuu alionao kwenye maisha yake.

Hatua ya kuchukua;
Jua mkondo wako kwenye fedha na mafanikio ni upi, kisha kazana kwanza kubadili mkondo huo.
Kujua mkondo wako, angalia matokeo ambayo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara kwako. Kama kila wakati unakuwa kwenye madeni na kipato kutokutosheleza, huo ndiyo mkondo wako. Kabla hujakimbilia kuongeza kipato, badili kwanza mtazamo mzima ulionao kifedha.
Maama huo ndiyo unaoathiri sana matokeo ya mwisho kuliko hata hatua unazochukua.

Tafakari;
Kile ambacho watu wanaita hatima ya maisha nj mtazamo wa ndani ambao ndiyo unaathiri maisha yote ya mtu. Uzuri ni kila mtu anayo nguvu ya kubadili mtazamo huo wa ndani. Hiyo ina maana kwamba kila mtu anayo nguvu ya kubadili hatima ya maisha yake.
Kwa maana hiyo basi, hapaswi kukubali kwamba maisha yako ndivyo yalivyo na huna cha kufanya.
Unayo mengi ya kufanya, ukianza na kubadili mtazamo wako wa ndani.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed