2953; Fanya machache kufanya makubwa.

Rafiki yangu mpendwa,
Huwa tunadhani ili tuweze kufanya makubwa, basi tunahitaji kufanya mambo mengi sana.
Hilo linapelekea tujihangaishe na mambo mengi na mapya kila wakati.

Lakini cha kushangaza, hata baada ya kuhangaika na mengi, bado matokeo tunayoishia kupata ni ya kawaida sana.

Tunahangaika na mengi, tunachoka sana na mwishowe hakuna tunachoambulia.

Ili tuweze kuzalisha matokeo makubwa, tunachohitaji siyo kufanya mambo mengi.
Bali tunapaswa kufanya machache yaliyo muhimu kabisa na kuyafanya kwa kina.

Unapofanya mengi, unakutana na usumbufu mwingi ambao unapunguza sana ubora wa kile unachofanya.

Unapofanya mengi, unafanya kwa juu juu badala ya kuzama ndani kwa kina.

Unapofanya mengi, unakuwa bize sana, kitu kinachopelekea yale muhimu zaidi yakose nafasi ya kufanyika.

Kuondokana na changamoto hizo, unapaswa kufanya maamuzi ya makusudi kabisa ya kufanya machache ili uweze kufanya makubwa.

Anza kwa kuorodhesha malengo makubwa uliyonayo, kulingana na umuhimu wake. Kisha chagua malengo matatu ya juu na hayo ndiyo unayoyawekea nguvu zako zote kwa sasa.

Kisha orodhesha mambo yote ambayo umekuwa unayafanya kwenye kila siku yako. Weka yote kabisa bila kuacha hata moja.

Sasa basi, oanisha yale unayofanya na mchango wake kwenye malengo makuu matatu. Angalia ni yapi unayofanya ambayo yanachangia kwenye malengo makuu matatu.

Yale tu yenye mchango kwenye malengo makuu matatu uliyochagua kuyawekea umakini ndiyo utapaswa kuendelea kuyafanya kwa sasa.
Mengine yote utapaswa kuacha kuyafanya kwa sasa.

Kwa kupunguza mengi unayofanya, utapata muda zaidi na umakini zaidi wa kuweka kwenye machache uliyochagua.
Bado utapata tamaa ya kuanza mengine mapya utakayoona ni bora zaidi.

Lakini usidanganyike kwa hayo, baki kwenye yale machache uliyochagua kuwa ndiyo muhimu na yafanye kwa kina kabisa.
Hivyo ndivyo mafanikio makubwa yanavyotengenezwa.

Tofauti ya wanaofanikiwa na wanaoshindwa haipo kwenye nini wanachofanya, bali ipo kwenye namna wanavyofanya kile wanachofanya.

Wanaofanikiwa sana wanajua kwa kina kile wanachofanya na wanafanya kwa viwango vya juu sana.
Hilo linawatenga na wengine hivyo kupata fursa nzuri na kubwa.

Wasiofanikiwa wanajua kwa juu juu kile wanachofanya na wanafanya kwa hovyo na mazoea. Hilo linafanya wawe kwenye kundi kubwa la wafanyaki wa kawaida kitu kinachowaweka kwenye ushindani mkubwa.

Kama hakuna kitu ambacho watu wanakipata tofauti kwako, hakuna makubwa unayofanya.
Kama hakuna kitu ambacho watu wanaweza kukipata kwako tu na hakuna pengine wanaweza kupata dunia nzima, watu hawatakuwa na sababu ya kuacha wengine na kuja kwako.

Mara nyingi kukimbilia kufanya mambo mengi ni njia ya kuficha uvivu na uzembe ulio ndani ya mtu.
Mtu anakuwa hayupo tayari kuweka juhudi kubwa zinazohitajika kwenye kitu, kwa kukifanya kwa kina.
Hivyo anakimbilia kufanya mengi yasiyokuwa na tija.
Anachotaka ni aonekane tu yupo bize.

Ingekuwa kuwa ‘bize’ ndiyo kuwa na mafanikio, kila mtu angekuwa tayari ana mafanikio makubwa.
Maana hakuna kipindi ambacho watu wapo ‘bize’ kama sasa.
Lakini matokeo yanajidhihirisha yenyewe, pamoja na watu kuwa bize sana, matokeo hayaridhishi.

Wewe ondoka kwenye huo mkumbo, usikimbilie tu kuwa ‘bize’, badala yake angalia ni hatua zipi za tofauti unazopiga.

Mwanafalsafa Seneca aliwahi kusema tatizo siyo kwamba tuna muda mchache, bali tatizo ni tunao muda mwingi mpaka tunaishia kuutumia vibaya. Na hilo linajidhihirisha na jinsi wengi wanapenda kuwa ‘bize’.

Mahali pengine Seneca pia akasema; siyo kwamba hatufanyi kwa sababu mambo ni magumu, bali mambo ni magumu kwa sababu hatufanyi.
Kuhangaika na mambo mengi mapya ni kuacha kuweka juhudi kubwa kwenye machache muhimu.
Na mwishowe tunalalamika mambo ni magumu, hiyo ni kwa sababu hatufanyi yaliyo muhimu na kwa kina.

Pale unapojikuta unasema upo ‘bize’ na huna muda wa kufanya mambo unayojua ni muhimu, ndiyo wakati wa kufumbuka macho na kupunguza hayo mambo unayofanya.

Mwisho wa siku hautahesabiwa kwa mengi uliyofanya, bali utahesabiwa na makubwa uliyofanya.
Weka kipaumbele chako kwenye makubwa na siyo mengi.
Ukubwa utakupa mengi unayotaka, wakati mengi yakikukosesha ukubwa huo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe