Rafiki yangu mpendwa,

Misingi ya karibu dini na falsafa zote inatuambia kitu kimoja, tumeumbwa kwa mfano wa Mungu. Na kama ndivyo, basi ndani yetu tuna sifa za uungu. Na ni sifa hizi ndizo zinazotuwezesha kufanya makubwa sana kwenye maisha yetu.

Mungu ana sifa kuu tatu;

Moja ni muweza wa yote, hakuna chochote kinachomshinda.

Mbili ni mjuzi wa yote, hakuna asichojua.

Tatu yupo kila mahali, hakuna asipokuwa.

Kwa kuwa sisi tumeumbwa kwa mfano wake, basi pia tuna sifa hizi kuu tatu, tunaweza kufanya chochote, pia tunaweza kujua chochote na tunaweza kuwa kila mahali.

Unaweza kujiuliza hilo linawezekanaje? Na jibu ni rahisi, tunaweza kuyafanya hayo matatu kwa kutumia nguvu kubwa sana iliyopo ndani yetu ambayo ni FIKRA ZETU.

Fikra zetu zinatuwezesha kufanya chochote tunachotaka kufanya, zinatuwezesha kujua chochote tunachotaka kujua na zinatuwezesha kuwa kila mahali.

galaxybrain

Unaweza kujiuliza fikra hizi hizi ambazo unakuwa nazo kila siku zinaweza kuwa na nguvu hiyo kweli? Kwamba fikra ulizozizoea kila siku, fikra unazotumia kuwaonea wivu wengine na kuwa na hofu na maisha zikuwezeshe kupata kila kitu?

Majibu ni ndiyo, fikra hizo hizo ukizitumia vizuri na kwa kuzitawala vyema, utaweza kufanya makubwa sana.

Fikra ni namna ambayo akili zetu zinafanya kazi. Sasa akili zetu zimegawanyika kwenye sehemu kuu mbili.

Sehemu ya kwanza ni akili yenye utambuzi au kwa kiingereza CONSCIOUS MIND, hii ni akili ambayo ina utambuzi wa mambo na kujua kila unachofanya. Ni akili ambayo unaweza kuidhibiti na kuisimamia utakavyo.

Sehemu ya pili ni akili isiyo na tambuzi au kwa kiingereza SUBCONSCIOUS MIND, hii ni akili ambayo haina utambuzi wa mambo na kujua kinachofanyika. Akili hii huwa inafuata masharti ya akili yenye utambuzi. Hii ni akili ambayo huwezi kuidhibiti moja kwa moja, na inafanya kazi muda wote.

Sasa kitu ambacho kinaweza kukushangaza kujua ni kwamba, maisha yako yanaendeshwa kwa asilimia 10 ya akili yenye utambuzi na asilimia 90 ya akili isiyo na utambuzi.

Akili isiyo na utambuzi ndiyo yenye nguvu kubwa ya kutupatia chochote tunachotaka. Hii ndiyo akili inayotuwezesha kujua kila kitu kwa sababu huwa hailali wala kupumzika. Vitu ambavyo umevisahau kwenye akili yenye utambuzi, havisahauliki kabisa kwenye akili isiyo na utambuzi, vyote vimehifadhiwa.

Kadhalika akili hii isiyo na utambuzi inatuwezesha kuwa kila mahali, kwa sababu inatuunganisha na watu wengine kupitia fikra ambazo tunazo na wengine wanazo. Unapokuwa na fikra fulani zinazotawala akili yako yenye utambuzi, akili isiyo na utambuzi inakuletea wale watu ambao wana fikra kama za kwako.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; THE HEALING POWER OF MIND (Nguvu Ya Tahajudi Kwenye Afya, Uzima Na Uamsho)

Hii ndiyo nguvu kubwa sana ambayo unayo ndani yako, ambayo unaweza kuitumia kupata chochote unachotaka.

Swali kuu linabaki, je unawezaje kutumia nguvu hii ya fikra na akili kupata chochote unachotaka? Na majibu ni rahisi na yapo wazi kabisa;

  1. Dhibiti akili yako yenye utambuzi, kwa kuweka fikra za kile ambacho unakitaka, mara zote fikiria kile ambacho unataka tu, na siyo usichotaka. Kadiri unavyofikiria kitu kwa muda mrefu, ndivyo akili isiyokuwa na utambuzi inajua ni kitu muhimu na kukuweka kwenye mazingira ya kukipata.
  2. Fikiria kwa namna chanya na kama tayari umeshapata kile unachotaka. Akili isiyo na utambuzi huwa haiwezi kutofautisha kitu halisia na kisicho halisia, yenyewe huwa inafanya kazi kutokana na fikra ambazo zimetawala akili yenye utambuzi kwa muda mrefu. Hivyo unapoweka fikra chanya na za umiliki, akili hiyo inajua kwamba tayari unacho kile unachotaka na hivyo kuendelea kukupatia.
  3. Tengeneza picha ya kiakili ya kile unachotaka, na itafakari picha hiyo mara kwa mara. Jione ndani ya picha hiyo, ona kabisa kama tayari una kile unachotaka. Kama ni gari jione ukiwa ndani ya gari hiyo, kama ni nyumba jione uko ndani ya nyumba hiyo. Akili zetu zinaelewa picha haraka kuliko maelezo, hivyo unapotumia taswira, akili isiyo na utambuzi inahakikisha huo ndiyo unakuwa uhalisia wa maisha yako.
  4. Usiruhusu mawazo pinzani kuingia kwenye akili yako, na yakiingia kwa bahati mbaya yang’oe haraka kabla hayajaleta madhara. Ukishajua unachotaka, ukishatengeneza taswira yako kiakili, usiwe na wasiwasi iwapo utafikia au la, kuwa na uhakika utafikia, usiruhusu kabisa wazo lolote hasi kuingia kwenye akili yako, usiyape nafasi mawazo yanayopingana na kile unachotaka yaingie kwenye akili yako. Na ikitokea yameingia kwa bahati mbaya, yang’oe haraka sana kabla hayajaweka mizizi na akili isiyo na utambuzi kuyafanyia kazi.
  5. Jipe muda, hakuna kitu kinachotokea haraka, ukishaweka fikra zako vizuri, achia kazi akili isiyo na utambuzi ikamilishe. Wewe weka juhudi kwenye kila unachofanya, piga hatua zaidi na usiwe na haraka. Usilazimishe vitu vitokee kwa namna unavyotaka au wakati unaotaka. Jiwekee muda wa kupata unachotaka na iache akili isiyo na utambuzi ifanyie kazi, ndani ya muda huo utapata unachotaka, lakini siyo kwa kulazimisha.

Rafiki, fikra na akili ndiyo nguvu kubwa sana iliyopo ndani yako na unayoweza kuitumia kupata chochote unachotaka. Tumia vizuri akili na fikra zako kuweza kufanya makubwa kwenye maisha yako. Fanyia kazi hatua tano ulizojifunza hapa na utaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.

Huenda dhana uliyojifunza hapa ikawa ngumu kwako kuelewa kwa haraka, nashauri usome taratibu na kurudia tena na tena na tena huku ukiwa umefungua fikra zako kwa lengo la kujifunza na utajifunza na kuona hatua za kuchukua.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge