3085; Hamasa na kufanya.

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna kitendawili kikali sana kwenye hamasa na kufanya kama ilivyo kwenye yai na kuku.
Watu huwa wanatumia muda mwingi kujadiliana kipi kilianza kati ya yai au kuku.
Inakuwa kitendawili kikali kwa sababu ukisema yai lilianza, utaulizwa lilitagwa na kuku yupi?
Na ukisema kuku alianza, utaulizwa kutoka kwenye yai gani?
Ukweli wa kitendawili hicho ni chochote kinaweza kuwa kilianza na haileti tofauti yoyote.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye hamasa na kufanya.
Watu wengi huwa wanasubiri mpaka wapate hamasa ndiyo wafanye kile walichopanga kufanya.
Halafu kwa bahati mbaya sana, hiyo hamasa haiji na hivyo wanajikuta wakisubiri kwa muda mrefu bila kufanya.

Ukweli ni kwamba, hamasa na kufanya vibakwenda pamoja, kila kimoja kikiweza kumchochea mwenzake.
Kama huna hamasa ya kufanya, hupaswi kusubiri mpaka hamasa ije ndiyo uanze kufanya.
Badala yake unatakiwa uanze kufanya hivyo hivyo na utaweza kujijengea hamasa ya kuendelea kufanya.
Kwa kufanya, unachochea hamasa inayokuwezesha kuendelea kufanya zaidi.

Kama wakati wowote ule utaamua kuamka na kuanza mwendo, maisha yatafunguka sana kwako.
Lakini kama utasubiri mpaka uwe na hamasa ndiyo ufanye, kamwe hutaweza kuanza.

Hamasa huwa ni zao la kufanya kama ambavyo kufanya pia ni zao la hamasa.
Hivyo kila unapokuwa na wasiwasi wa aina yoyote ile, anza kufanya kitu chochote kile.
Kila unapojiona huna hamasa, anzisha mwendo wowote ule.
Kwa kuwa kwenye mwendo, utaweza kubadili hali yako kutoka kutokuwa na hamasa mpaka kuwa na hamasa.

Usisubiri mpaka uwe na hamasa ndiyo ufanye yale uliyopanga kufanya.
Badala yake anza kufanya na hilo litakujengea hamasa ya kuendelea kufanya.

Kama ilivyo kwa kanuni ya mwendo, kitu kilichosimama huwa kinaendelea kusimama na kilicho kwenye mwendo huwa kinaendelea na mwendo.
Usikubali kusimama kwa sababu yoyote ile.
Mara zote endelea kuwa kwenye mwendo, hilo litajenga hamasa kubwa kwako itakayoendelea kukusukuma kuwa bora zaidi ya ambavyo upo sasa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe