Kila mtu anapenda kuwa tajiri ama kufanikiwa kifedha katika maisha. Kila mtu anahangaika kila siku ili kuweza kufikia malengo hayo. Katika mahangaiko hayo kuna watu wanaotafuta ‘short cut ’ ama njia fupi ya kufikia malengo hayo. Je ni kweli kuna njia fupi za kufikia mafanikio yako? Jibu ni ndio zipo njia nyingi fupi za kufikia malengo yako, tena zipo nyingi sana. Zipo ambazo ni njia halali na nyingine sio halali.
    Kuna njia nyingi za kupata fedha kwa haraka, baadhi ya njia hizo ni wizi, ufisadi, dhuluma, kushinda bahati na sibu, kurithi na kadhalika. Tatizo kubwa la njia hizi ni kwamba mafanikio yanayopatikana huwa hayadumu. Mtu anaweza kupata fedha nyingi sana kwa njia hizo ila huwa hazidumu. Fedha hizi hazidumu kwa sababu fedha ina tabia moja ya ajabu ambayo wengi tunashindwa kuielewa. Kuna sayansi ya kupata fedha, kutumia fedha na kuilinda fedha isipotee. Wengi tunajua jinsi ya kupata fedha, iwe halali au haramu. Namna ya kutumia fedha wengi tunaendeshwa na fedha, na kuilinda isipotee hapo ndio pagumu sana kwa watu wengi.
   Fedha ambayo haijapatikana kwa mipango na malengo fulani ni rahisi sana kutumia na ni ngumu sana kulinda. Kwa mfano sasa hivi hapo ulipo ukipewa shilingi bilioni moja utazifanyia nini? Kama hujawahi kuwa na mpango wa kupata bilioni moja na kuwa na mkakati wa jinsi ya kuitumia utajikuta unafanya mambo ya ajabu sana. Ila ukipewa milioni moja au kumi ambazo umekuwa ukizifikiria kila siku unaweza kuzitumia vizuri na ukafika bilioni moja na hata zaidi.
  Kuna uhusiano mkubwa wa kisaikolojia wa matumizi ya fedha na jinsi ilivyopatikana. Fedha iliyopatikana kwa kazi ngumu huwa inatumika kwa makini sana. Fedha iliyopatikana kirahisi na kwa mkupuo huwa inatumika hovyo na hivyo kuisha haraka. Sote ni mshahidi, wapo watu wengi waliopata fedha nyingi kwenye bahati na sibu, mirathi ama kwa dhuluma. Ila wengi wao waliishia wapi?
   Tunaweza kusema kuna njia rahisi za kupata utajiri wa haraka, ila hakuna njia rahisi za kupata utajiri wa kweli udumuo na utakaokupatia amani ya nafsi yako. Kama unataka kupata utajiri udumuo, ambao kila mtu anaweza kama akitaka, fanya kazi kwa bidii na maarifa, pia kuwa mbunifu kila mara. Usikate tamaa unapokutana na vikwazo, kila mtu anakutana navyo. Usipoteze muda kutafuta njia za kutajirika haraka, hazitakufikisha mbali.