Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza njia bora kabisa ya kumaliza umbea na majungu katika maisha yako hivyo basi,  karibu tujifunze.

Kama ni ugaidi mkubwa ulioibuka katika jamii yetu basi ni ugaidi wa umbea yaani terorism of gossips, huu ni ugaidi hatari sana katika maisha yetu. umbea unawajeruhi watu na kuwasababishia majeraha ya moyo kadiri ya Papa Francis ‘’ wakati dunia inapombana na magaidi katika jumuiya zetu hatuna budi kupambana na magaidi wa umbea, masengenyo, udaku, majungu, manyanyaso, dhuluma ambayo yamejeruhi na hata kuwaua wengi kiroho, kisaikolojia, kijamii na kihisia.’’

umbeya

Kumbe basi, ugaidi wa umbea na majungu ‘’  ni ugaidi hatari na mbaya zaidi kuliko hata ule wa maangamizi ya mabomu wanaotumia boko haramu, alkaida, alshabau na wengine wa aina hiyo.’’ Silaha ya umbea na majungu ni hatari sana katika maisha ya binadamu kwani inawaangamiza watu wazima na kuwaua kabisa. Kazi ya umbea ni kazi ya watu waliokosa kazi ya kufanya kabisa huwezi kuanza kujeruhi watu kwa kuanza kumwaga sumu kwa kutumia ulimi wako kama una kazi ya kufanya.

Rafiki, ulimi ni kiungo hatari kinachomwaga sumu sana na kama tukisema kiungo kilichojaa laana na uchafu basi ni ulimi kwani kinatoa kila aina ya maneno unayoyajua wewe. Tunaposhindwa kutawala ndimi zetu ndipo tunakaribisha hatari kubwa katika jamii yetu na jamii ya leo inapenda habari za umbea kuliko kazi na hii ni hatari kabisa hata kwa ustawi mzima wa maendeleo binafsi na hata ya taifa kwa ujumla.

Mimi leo ninakuletea suluhisho la umbea kabisa katika kujisomea kwangu kwa watu walioacha mawazo katika vitabu na walioweza kuishi karne  za nyuma kabisa nikakutana na maneno haya ya Mt Maria Magdalena wa Pazzi akisema, ‘’ usiseme hata mara moja kuhusu mwingine, kile ambacho hutathubutu kusema akiwepo mwenyewe. Wasemee wengine yale upendayo wakusemehe wewe’’

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoamua Kuharibu Maisha Yako Mwenyewe Bila Ya Kujua.

Rafiki, kama kila mmoja wetu ataweza kuyaweka maneno hayo akilini basi tutapunguza kama siyo kumaliza kabisa matatizo ya umbea na majungu kwani imekuwa ni kero kubwa katika jamii yetu. watu wanajeruhiana maeneo ya kazi zao na hata kufikia kipindi cha kukinai hata mazingira ya kazi yake na kuona hana thamani pale, umbea na majungu yanawaumiza watu zaidi kuliko hata hayo mashambulizi tunayoyasikia ya mabomu.

Hatua ya kuchukua leo, usiseme hata mara moja kuhusu mwingine, kile ambacho hutathubutu kusema akiwepo mwenyewe. Wasemee wengine yale upendayo wakusemehe wewe’’ achana na biashara hii ya umbea kwani haina faida fanya biashara bora ya kutoa  ni upendo kwa wengine na kujali maisha yako.

Kwahiyo, umbea na majungu ni moja ya kemikali hatari inayoua watu wengi katika jamii yetu na watu wengi wamedhoofika kiakili kwa sababu ya maneno yenye sumu kama haya. Kinywa chako ukikitumia vizuri ni faida lakini ukikitumia vibaya ni kama sumu ya kobra ambayo inamaliza watu mara moja. Ili tuweze kuibadilisha dunia tunaalikwa kuanza kubadilisha sisi na mimi leo nimeanza kukubadilisha dunia kwa kuacha kufanya tabia hii ya aibu na hatari kwa maisha yetu.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net  au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi kila siku. Asante sana